Powered By Blogger

Friday, April 6, 2012

UJIO WA PROF. A. ABDALLA UDSM, TANZANIA

Ni mmoja ya mwanafasihi, mpenzi wa lugha adhwim na aula ya kiswahili niliyotokea kumhusudu katika ujana wangu hasa tangu niingiwe na mdudu wa kukipenda na kukienzi kiswahili.
Si mwingine bali ni yule mshairi, mhadhiri na mtangazaji Profesa Abdilatif Abdalla kutoka Mombasa, Kenya aliyewahi kufungwa jela kuanzia mwaka 1969-1972 katika gereza la Kibiti nchini Kenya baada ya serikali ya Jomo Kenyatta kumtia hatiani eti kisa aliandika ukweli kuhusu hofu na wahaka dhidi ya uongozi wake katika kabrasha la Kenya Twendapi.
Profesa Abdala atakuwepo nchini Tanzania akitokea nchini Ujerumani alikokua akifundisha lugha ya kiswahili katika Chuo Kikuu cha Leipzig katika mhadhara utakaofanyika katika Chuo Kikuu kikongwe cha Dar-Es-Salaam. Akiwa kama mmoja wa wahadhiri siku hiyo ya Ijumaa ya tarehe 13, Aprili mwaka huu katika ukumbi wa Nkrumah, Osagefyo, Profesa atachimba hasa na kutoa vumbi dhidi ya mchango kuntu unaotolewa na wasanii katika ukombozi wa bara la Afrika.
Profesa Abdilatif Abdalla 
Mhadhara huo utaanza rasmi saa 2 asb ila Gwiji mwenyewe atapamba na kuling'arisha jukwaa majira ya saa 3 unusu.

Wote mnakaribishwa.

2 comments:

  1. Duuuuuuuu...mbona sikujua hili? Maana ningepitia kitabu chake "Sauti Ya Dhiki" kitoke wakati akiwa nchini- ndo nimemaliza kukisoma baada ya miaka takriban 35. Nilikisoma mara ya kwanza nikiwa kijana sana- sikukielewa na sasa nakielewa zaidi- maana kinathibitisha haiba ya Viswahili vya aina nyingi tulivyo navyo ikizingatia vile vile maudhui ya siasa zetu Afrika.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Katika kitabu chake cha Sauti Ya Dhiki Shujaa huyu wa Kimvita ni pale antoneshapo hisia zangu kwa ndugu zangu walionitoka hasa lile shairi la Mi Nawe Mbali Tungawa si mchezo ama kweli kweli Allah hujalia waja wake kwa kila hali, ukikosa pesa utapewa ujasiri, akili, busara, weledi, umbuji wa mambo, talanta n.k basi kama ni ukwasi basi Sheikh Abdillatif kashaijishwa na kitu u Bill Gates wa Lugh'a!!! Najua unacho kitabu tena kina jalada la rangi nyekundu hebu litalii tena shairi Uncle Matcha...

      Delete