Powered By Blogger

Sunday, April 15, 2012

MAREHEM KANUMBA NA FUNZO KWA VIJANA TANZANIA

Marehem Steven Charles Kanumba ( 1984-2012)
Tarehe 7 Aprili mwaka 2012, itakuwa siku ya kukumbukwa sana hasa kwa waigizaji wa filamu Tanzania almaaruf Bongo Movies baada ya kumpoteza kipenzi na msanii mwenzao Steven Charles Kanumba.
Marehem Steve aliyependa kujiita The Great lenye maana sawa na Wonderful au maridhawa kwa lugha ya kiswahili chepesi kitu kizuri, shani, kupendeza na thamani kifupi Shujaa.
Jina hilo la utani halikuacha kuwa sanjari na mjiitaji husika, kwani hakuwa maridhawa tu bali alipanda maghorofa kadhaa ya juu.
Tathmini ya namna ya uigizaji wake, vituko, mizaha yake iliyonakshiwa na haiba jamali aliyoshaijishwa na Malik.
Maandishi hayatoshi kumuelezea kama mwigizaji, matayarishaji na mwanamuziki alikuwa na talanta ya pekee kwa watanzania pamoja na waafrika kiujumla.
Filamu ni moja ya sanaa ya kipekee duniani ambayo ndani yake utakuta kila makabila kadhaa ya sanaa kama muziki, fasihi, ususi, ufumaji, uchoraji n.k.
Sinema alizowahi kufanya marehem zinakadiriwa kufika mia moja (100) zilikuwa na zitakuwa zikimuanika na kumuonyesha kuwa alichukulia sanaa ile kama uwanja ambao angeweza kuutumia zaidi kuelimisha na kuitangaza jamii yake hata kimataifa.
Katika filamu zake aliweza kusadifu mambo mengi yanayowazuzua waafrika wengi hasa sula la mapenzi, ugumu wa maisha pamoja na upotoshwaji na usahaulifuwaji wa mila na desturi za kitanzania.
haitoshi kuwaanika wanawake wakiwa nusu uchi waliojawa na ubinafsi sura na taswira iliyopo kwa wasichana wengi wa kitanzania.
Hakuwa tu msanii yule aliyetakwa na jamii bali yeye ndo alijikaramia kwa jamii yake hasa. Kauli yake ya kuwa aliichukulia tasnia hiyo kama baba na mama yake ilijidhihirisha katika uwezo wake wa kubuni, kuigiza na hata namna ya kufikisha ujumbe katika jamii yake.
Kifo cha nyota huyu ni pigo kimeacha pengo kubwa katika sanaa ya tanzania kijumla kwani hakujifungisha ndoa tu na filamu bali na muziki vilevile.
Kanumba anatoa mafunzo kama kijana aliyekataa kusema hapana na aliyeshinda kulala kwa kuridhika na mafanikio aliyowahim kuyapata. Kitendo cha kushirikiana na waigizaji kutoka nigeria ni ishara tosha kuwa shujaa huyu alijiona hajafanya lolote kwa jamii yake hivyo daima alijiona yu njiani.
Alikuwa mchapakazi hasa kwani si ajabu kuona ushiriki wake katika kipengele zaidi ya kimoja katika sinema alizowahi kufanya. Suala la kuwa hata balozi wa star times pia ni elimu kwani tanzania ina wasanii wangapi lakini kwanini kampuni ile ilimuomba kuwa taswira ya matangazo ya bidhaa zao ambayo bado aliing'arisha.
yumkini hata kama haitoshi kuwa mwakilishi wa shirika la misaada ya Uingereza la Oxfam nichini Tanzania bado inashawishi kuwa ama hakuna anayepinga kuwa taifa limempoteza kijana aliyejua wapi anatoka na wapi anaelekea.
Aliyewahi kuwa bondia maarufu duniani Muhammad Ali aliwahi kusema kuwa ni vigumu kuwa mnyenyekevu kwa watu hasa kama utakuwa shujaa kama yeye. Muhammad ni mtu mpole sana pamoja na historia ya ajabu aliyoweka katika ulingo duniani lakini bado aliithamini na kuisikiliza jamii yake kinyume na baadhi ya watu wakishapanda vichuguu kidogo basi hujawa na viburi, dharau, majivuno, tambo na tadi na kejeli kwa walimwengu wenzao.
Marehemu Kanumba anaingia katika tabaka la watu ambao wala hawakuwahi kuingiwa kichwani na umaarufu kwani alikuwa mpole, msikivu, mwenye aibu ya wastani, hekima na busara sifa ambazo waeza kuziona kupitia hata alipokuwa akifanyiwa mahojiano katika vituo mbalimbali vya runinga hapa nchini.
chanzo cha kifo chake kimezua mjadala na sura picha mbaya miongoni mwa watanzania japo kuna hatua ambayo wengi tunaisahau kuwa hakuna hata mtu mmoja katika dunia anayejua namna atakavyokufa ama kurejea kwa Bwana Muumba. laiti tungekuwa tunajua namna tutakavyofariki hakika hakuna kiumbe yoyote angethubutu kujishughulisha na jambo lolote la kimaendeleo bali kuwazia namna atakavyoikabili siku hiyo.
Si lazima kuangalia ubaya wa mtu au wa kitu, marehemu Kanumba katuachia changamoto nyingi sana sisi vijana wa kitanzania, tujaribu kutathmini uzuri na mchango aliojaaliwa kuufanya kwa taifa la tanzania ili mimi, yule, wewe, wao hatuna budi kifikiria namna na sisi tutakavyoweza kukumbukwa kama vijana tuliojaribu kuifanya jamii yetu iache kuishi inavyoishi na kuishi namna inavyopaswa kuishi.

BASATA haina budi kumuenzi Marehem Kanumba hata kwa kumfungulia wakfu ( Foundation ) utakaokumbuka yale yote aliyoyahimiza katika kuendeleza sanaa ya uigizaji Tanzania. Hata tovuti maalum itakayohifadhi falsafa zake dhiki ya kukwamua uwanja huo wa burudani nchini, tovuti hiyo iwe na picha, vidio zake na mahojiano yake kama urithi kwa kizazi kitakachokuja ili kumuenzi na kumkumbuka Baba huyu wa Filamu Tanzania.

"Watu wenye vipaji ndio hufanikiwa maishani lakini kati ya hao ni wale wachapakazi tu"- Quincy Jones Jr, mtayarishaji, mwelekezaji na mpangaji wa muziki nchini Marekani .

1 comment:

  1. Maoni mazuri sana-ama kweli Kanumba alitimiza kazi iliyomleta duniani. Halafu pia ni raha iliyoje kuona blogu lililoandikwa katika Kiswahili fasaha- maana mabloga na waandishi wengi chipukizi siku hizi hawazingatii utajiri wa lugha yetu- kazi yao kukopa kopa na kuazima maneno ya Kiingereza- utadhani lugha yetu hii tukufu na tajiri haijitoshelezi. Tangu lini ukamwona Mwingereza mwenyewe au Mfaransa akabandika maneno ya mwenzake- anaweza kupachika msemo mmoja- lakini haiwi ndiyo kauli, mila na desturi. Nakupongeza Bakari Msuya

    ReplyDelete