Powered By Blogger

Saturday, April 28, 2012

KWANINI
HABA NA HABA BBC Swahili NA SI TBC Taifa?

Kipindi maridhawa kilichoanzishwa tarehe 24 machi na Idhaa ya Kiswahili BBC cha Haba Na Haba ( Little by Little) hakina budi kunizushia mjadala binafsi ya kuwa kwa nini Shirika la Habari la Uingereza ndio limeweza kuchukua fursa na wasaa huo badala ya watanzania kuweza kutumia vyombo vyao vya habari kama TBC kuwa ndio daraja madhubuti la kupitishia malalamiko, vilio, mikasa, raha, furaha na shangwe zao kwa viongozi?

TBC na vyombo vingine vya habari nchini hhaviana uwezo wa kuwakutanisha watanzania na viongozi mpaka BBC watufanyie hatuwezi kuwa makini namna hiyo kwa mintaarafu ya kutafuta na kujua mstakabali wa taifa la tanzania kama tunashindwa kufanya jambo kama hili. hii ni dalili tosha kuwa ama kweli tanzania haina waandishi wabunifu kama ilivyo katika vyombo vingine vya habari kimataifa. hoja hii inaweza kushaijishwa na mlolongo wa vipindi vingi vya muziki si katika redio wala runinga ambavyo dhima yake kubwa ni kuburudisha tu na kumfanya mwananchi wa kawaida ashindwe kukaa na kutathmini namna atakavyoweza kupambana na mabadiliko haya ya kidunia, kukua kwa kasi kwa sayansi na teknolojia, mabadiliko ya tabia nchi, ongezeko la watu duniani, uharibifu wa mazingira na majanga mbalimbali. Si redio wala Runinga ambayo imethubutu kuandaa vipindi aushi kwa kuielimisha jamii namna ya kuja kupambana na changamoto za Muungano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, la hasha...

Vyombo vya habari huchukuliwa kama ndio nguzo ya nne katika mfumo wa uongozi nchini ukiongozwa na serikali kuu, bunge na mahakama japo Msomi mwenye kuhusudu siasa za wastani, mwanasheria na mwandishi Profesa Issa Shivji hasiti kuviweka angani vyomo hivyo kuwa ni nguzo ya kwanza kwa mintaarafu ya maslahi ya jamii. Kipindi cha Haba na Haba huangazia mashakili mengi yanayowasibu watanzania na kujaribu kuyafikisha mateso hayo kwa wawakilishi wao kuanzia ngazi ya kijiji hadi ya taifa. Tangu kianzishwe kimeanika matatizo mbambali nchini tena yaliyopo mbali na jiji la Dar-es-Salaam kama tatizo la maji, vitanda hospitalini, vifaa, madarasa pamoja na walimu katika shule za msingi nchini pamoja na tatizo miundombinu. Haya ni masahibu makubwa mno ambayo si kweli kuwa kama taifa la Tanzania lingekuwa na viongozi wote wazalendo kama walivyo baadhi suluba hizi zisingepungua kwa asilimia zaiidi ya sabini. Ukichimba sana utagundua kuwa haya masuala yote yanatatulika ikiwa kutakuwa na UTAWALA BORA ambao ndio dhamira kuu ya kipindi cha haba na haba. Neno utawala au uongozi bora ni kama vile halipo si tu katika kamusi ya TUKI bali hata katika vitabu tukufu vya Injili, Qur'an na Biblia kwa viongozi wa kiafrika...

Haba na Haba ni moja ya kipindi kinchoamsha na kuwaletea changamoto waandishi wa kitanzania kuwa hawana budi kukaa chini na kuanzisha vipindi vyenye kuelimisha jamii ili kuweza kufikia malengo ya Milenia kama si kupiga hatua na kufikia nchi kama Indonesia, Singapore, Afrika Kusini na India kimaendeleo. Vyombo vya habari ni moja taswira inayosadifu uwezo wa fikra wa jamii fulani. Waandishi wekeni Utaifa mbele kwanza...

Mtangazaji wa kipindi hiko mujarab Hassan Mhelela amesema ana furaha kubwa kuwa sehemu ya kipindi hiko ambacho ni jukwaa la heshima la kuwawajihisha watanzania na viongozi.

Haba na Haba hutangazwa na BBC Swahili saa 10.05 alasir kwa saa za Afrika Mashariki, jumamosi na jumapili saa 12 asubuhi.Unaweza kukisikiliza kupitia tovuti ya bbcswahili.com.


No comments:

Post a Comment