Powered By Blogger

Saturday, April 28, 2012

KWANINI
HABA NA HABA BBC Swahili NA SI TBC Taifa?

Kipindi maridhawa kilichoanzishwa tarehe 24 machi na Idhaa ya Kiswahili BBC cha Haba Na Haba ( Little by Little) hakina budi kunizushia mjadala binafsi ya kuwa kwa nini Shirika la Habari la Uingereza ndio limeweza kuchukua fursa na wasaa huo badala ya watanzania kuweza kutumia vyombo vyao vya habari kama TBC kuwa ndio daraja madhubuti la kupitishia malalamiko, vilio, mikasa, raha, furaha na shangwe zao kwa viongozi?

TBC na vyombo vingine vya habari nchini hhaviana uwezo wa kuwakutanisha watanzania na viongozi mpaka BBC watufanyie hatuwezi kuwa makini namna hiyo kwa mintaarafu ya kutafuta na kujua mstakabali wa taifa la tanzania kama tunashindwa kufanya jambo kama hili. hii ni dalili tosha kuwa ama kweli tanzania haina waandishi wabunifu kama ilivyo katika vyombo vingine vya habari kimataifa. hoja hii inaweza kushaijishwa na mlolongo wa vipindi vingi vya muziki si katika redio wala runinga ambavyo dhima yake kubwa ni kuburudisha tu na kumfanya mwananchi wa kawaida ashindwe kukaa na kutathmini namna atakavyoweza kupambana na mabadiliko haya ya kidunia, kukua kwa kasi kwa sayansi na teknolojia, mabadiliko ya tabia nchi, ongezeko la watu duniani, uharibifu wa mazingira na majanga mbalimbali. Si redio wala Runinga ambayo imethubutu kuandaa vipindi aushi kwa kuielimisha jamii namna ya kuja kupambana na changamoto za Muungano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, la hasha...

Vyombo vya habari huchukuliwa kama ndio nguzo ya nne katika mfumo wa uongozi nchini ukiongozwa na serikali kuu, bunge na mahakama japo Msomi mwenye kuhusudu siasa za wastani, mwanasheria na mwandishi Profesa Issa Shivji hasiti kuviweka angani vyomo hivyo kuwa ni nguzo ya kwanza kwa mintaarafu ya maslahi ya jamii. Kipindi cha Haba na Haba huangazia mashakili mengi yanayowasibu watanzania na kujaribu kuyafikisha mateso hayo kwa wawakilishi wao kuanzia ngazi ya kijiji hadi ya taifa. Tangu kianzishwe kimeanika matatizo mbambali nchini tena yaliyopo mbali na jiji la Dar-es-Salaam kama tatizo la maji, vitanda hospitalini, vifaa, madarasa pamoja na walimu katika shule za msingi nchini pamoja na tatizo miundombinu. Haya ni masahibu makubwa mno ambayo si kweli kuwa kama taifa la Tanzania lingekuwa na viongozi wote wazalendo kama walivyo baadhi suluba hizi zisingepungua kwa asilimia zaiidi ya sabini. Ukichimba sana utagundua kuwa haya masuala yote yanatatulika ikiwa kutakuwa na UTAWALA BORA ambao ndio dhamira kuu ya kipindi cha haba na haba. Neno utawala au uongozi bora ni kama vile halipo si tu katika kamusi ya TUKI bali hata katika vitabu tukufu vya Injili, Qur'an na Biblia kwa viongozi wa kiafrika...

Haba na Haba ni moja ya kipindi kinchoamsha na kuwaletea changamoto waandishi wa kitanzania kuwa hawana budi kukaa chini na kuanzisha vipindi vyenye kuelimisha jamii ili kuweza kufikia malengo ya Milenia kama si kupiga hatua na kufikia nchi kama Indonesia, Singapore, Afrika Kusini na India kimaendeleo. Vyombo vya habari ni moja taswira inayosadifu uwezo wa fikra wa jamii fulani. Waandishi wekeni Utaifa mbele kwanza...

Mtangazaji wa kipindi hiko mujarab Hassan Mhelela amesema ana furaha kubwa kuwa sehemu ya kipindi hiko ambacho ni jukwaa la heshima la kuwawajihisha watanzania na viongozi.

Haba na Haba hutangazwa na BBC Swahili saa 10.05 alasir kwa saa za Afrika Mashariki, jumamosi na jumapili saa 12 asubuhi.Unaweza kukisikiliza kupitia tovuti ya bbcswahili.com.


Sunday, April 15, 2012

MAREHEM KANUMBA NA FUNZO KWA VIJANA TANZANIA

Marehem Steven Charles Kanumba ( 1984-2012)
Tarehe 7 Aprili mwaka 2012, itakuwa siku ya kukumbukwa sana hasa kwa waigizaji wa filamu Tanzania almaaruf Bongo Movies baada ya kumpoteza kipenzi na msanii mwenzao Steven Charles Kanumba.
Marehem Steve aliyependa kujiita The Great lenye maana sawa na Wonderful au maridhawa kwa lugha ya kiswahili chepesi kitu kizuri, shani, kupendeza na thamani kifupi Shujaa.
Jina hilo la utani halikuacha kuwa sanjari na mjiitaji husika, kwani hakuwa maridhawa tu bali alipanda maghorofa kadhaa ya juu.
Tathmini ya namna ya uigizaji wake, vituko, mizaha yake iliyonakshiwa na haiba jamali aliyoshaijishwa na Malik.
Maandishi hayatoshi kumuelezea kama mwigizaji, matayarishaji na mwanamuziki alikuwa na talanta ya pekee kwa watanzania pamoja na waafrika kiujumla.
Filamu ni moja ya sanaa ya kipekee duniani ambayo ndani yake utakuta kila makabila kadhaa ya sanaa kama muziki, fasihi, ususi, ufumaji, uchoraji n.k.
Sinema alizowahi kufanya marehem zinakadiriwa kufika mia moja (100) zilikuwa na zitakuwa zikimuanika na kumuonyesha kuwa alichukulia sanaa ile kama uwanja ambao angeweza kuutumia zaidi kuelimisha na kuitangaza jamii yake hata kimataifa.
Katika filamu zake aliweza kusadifu mambo mengi yanayowazuzua waafrika wengi hasa sula la mapenzi, ugumu wa maisha pamoja na upotoshwaji na usahaulifuwaji wa mila na desturi za kitanzania.
haitoshi kuwaanika wanawake wakiwa nusu uchi waliojawa na ubinafsi sura na taswira iliyopo kwa wasichana wengi wa kitanzania.
Hakuwa tu msanii yule aliyetakwa na jamii bali yeye ndo alijikaramia kwa jamii yake hasa. Kauli yake ya kuwa aliichukulia tasnia hiyo kama baba na mama yake ilijidhihirisha katika uwezo wake wa kubuni, kuigiza na hata namna ya kufikisha ujumbe katika jamii yake.
Kifo cha nyota huyu ni pigo kimeacha pengo kubwa katika sanaa ya tanzania kijumla kwani hakujifungisha ndoa tu na filamu bali na muziki vilevile.
Kanumba anatoa mafunzo kama kijana aliyekataa kusema hapana na aliyeshinda kulala kwa kuridhika na mafanikio aliyowahim kuyapata. Kitendo cha kushirikiana na waigizaji kutoka nigeria ni ishara tosha kuwa shujaa huyu alijiona hajafanya lolote kwa jamii yake hivyo daima alijiona yu njiani.
Alikuwa mchapakazi hasa kwani si ajabu kuona ushiriki wake katika kipengele zaidi ya kimoja katika sinema alizowahi kufanya. Suala la kuwa hata balozi wa star times pia ni elimu kwani tanzania ina wasanii wangapi lakini kwanini kampuni ile ilimuomba kuwa taswira ya matangazo ya bidhaa zao ambayo bado aliing'arisha.
yumkini hata kama haitoshi kuwa mwakilishi wa shirika la misaada ya Uingereza la Oxfam nichini Tanzania bado inashawishi kuwa ama hakuna anayepinga kuwa taifa limempoteza kijana aliyejua wapi anatoka na wapi anaelekea.
Aliyewahi kuwa bondia maarufu duniani Muhammad Ali aliwahi kusema kuwa ni vigumu kuwa mnyenyekevu kwa watu hasa kama utakuwa shujaa kama yeye. Muhammad ni mtu mpole sana pamoja na historia ya ajabu aliyoweka katika ulingo duniani lakini bado aliithamini na kuisikiliza jamii yake kinyume na baadhi ya watu wakishapanda vichuguu kidogo basi hujawa na viburi, dharau, majivuno, tambo na tadi na kejeli kwa walimwengu wenzao.
Marehemu Kanumba anaingia katika tabaka la watu ambao wala hawakuwahi kuingiwa kichwani na umaarufu kwani alikuwa mpole, msikivu, mwenye aibu ya wastani, hekima na busara sifa ambazo waeza kuziona kupitia hata alipokuwa akifanyiwa mahojiano katika vituo mbalimbali vya runinga hapa nchini.
chanzo cha kifo chake kimezua mjadala na sura picha mbaya miongoni mwa watanzania japo kuna hatua ambayo wengi tunaisahau kuwa hakuna hata mtu mmoja katika dunia anayejua namna atakavyokufa ama kurejea kwa Bwana Muumba. laiti tungekuwa tunajua namna tutakavyofariki hakika hakuna kiumbe yoyote angethubutu kujishughulisha na jambo lolote la kimaendeleo bali kuwazia namna atakavyoikabili siku hiyo.
Si lazima kuangalia ubaya wa mtu au wa kitu, marehemu Kanumba katuachia changamoto nyingi sana sisi vijana wa kitanzania, tujaribu kutathmini uzuri na mchango aliojaaliwa kuufanya kwa taifa la tanzania ili mimi, yule, wewe, wao hatuna budi kifikiria namna na sisi tutakavyoweza kukumbukwa kama vijana tuliojaribu kuifanya jamii yetu iache kuishi inavyoishi na kuishi namna inavyopaswa kuishi.

BASATA haina budi kumuenzi Marehem Kanumba hata kwa kumfungulia wakfu ( Foundation ) utakaokumbuka yale yote aliyoyahimiza katika kuendeleza sanaa ya uigizaji Tanzania. Hata tovuti maalum itakayohifadhi falsafa zake dhiki ya kukwamua uwanja huo wa burudani nchini, tovuti hiyo iwe na picha, vidio zake na mahojiano yake kama urithi kwa kizazi kitakachokuja ili kumuenzi na kumkumbuka Baba huyu wa Filamu Tanzania.

"Watu wenye vipaji ndio hufanikiwa maishani lakini kati ya hao ni wale wachapakazi tu"- Quincy Jones Jr, mtayarishaji, mwelekezaji na mpangaji wa muziki nchini Marekani .

Friday, April 6, 2012

UJIO WA PROF. A. ABDALLA UDSM, TANZANIA

Ni mmoja ya mwanafasihi, mpenzi wa lugha adhwim na aula ya kiswahili niliyotokea kumhusudu katika ujana wangu hasa tangu niingiwe na mdudu wa kukipenda na kukienzi kiswahili.
Si mwingine bali ni yule mshairi, mhadhiri na mtangazaji Profesa Abdilatif Abdalla kutoka Mombasa, Kenya aliyewahi kufungwa jela kuanzia mwaka 1969-1972 katika gereza la Kibiti nchini Kenya baada ya serikali ya Jomo Kenyatta kumtia hatiani eti kisa aliandika ukweli kuhusu hofu na wahaka dhidi ya uongozi wake katika kabrasha la Kenya Twendapi.
Profesa Abdala atakuwepo nchini Tanzania akitokea nchini Ujerumani alikokua akifundisha lugha ya kiswahili katika Chuo Kikuu cha Leipzig katika mhadhara utakaofanyika katika Chuo Kikuu kikongwe cha Dar-Es-Salaam. Akiwa kama mmoja wa wahadhiri siku hiyo ya Ijumaa ya tarehe 13, Aprili mwaka huu katika ukumbi wa Nkrumah, Osagefyo, Profesa atachimba hasa na kutoa vumbi dhidi ya mchango kuntu unaotolewa na wasanii katika ukombozi wa bara la Afrika.
Profesa Abdilatif Abdalla 
Mhadhara huo utaanza rasmi saa 2 asb ila Gwiji mwenyewe atapamba na kuling'arisha jukwaa majira ya saa 3 unusu.

Wote mnakaribishwa.

Thursday, March 8, 2012

NANI KAMA MESSI KATIKA KANDANDA?

Lionel Messi akiwa na shujaa wake Maradona
Bado akiwa kinda wa miaka 24, Lionel Messi aweka rekodi ya kufunga magoli matano wakati klabu ya Barcelona ilipoicharanga Bayer Leverkusen magoli 7-1 wakati wa mehi ya marudiano wa kutafuta tiketi ya kucheza duru ya 16 bora ya mashindano hayo. Barcelona wameifunga Bayer Leverkusen jumla ya magoli 10-2 kufuatia ushindi wa kwanza walioupata dhidi ya wapinzani hao magoli 3-1 katika mzunguko mashindano hayo makubwa duniani.

Safu hii hasa ni kwa mintaarafu ya shabaab Messi ambaye katika msimu wa mwaka 2008-9 aliifungia timu yake magoli 9 na  mengine 8 msimu uliofuata na kuifungia magoli ithnaashara wakati Barcelona ilipotwaa vikombe viwili ndani ya misimu mitatu ya mashindano hayo.

Lionel Messi ameweka rekodi kwa kushika nafasi ya pili ya wafungaji wa juu kabisa katika mashindano hayo ambapo aliye kileleni ni Mjerumani Gerd Muller aliyewahi kufanya hivyo wakati mashindano hayo yakiitwa European Cup.

Mjerumani Gerd Muller
Gerd Muller aliyekuwa mshambuliaji hatari wa klabu ya Bayern Munich iliowahi kushinda vikombe vitatu vya Champions League miaka ya 70 ambapo mwaka 72-73 alifunga magoli 11, 73-74 na 74-75 akifunga magoli 8 kwa kila msimu.

Mreno kutoka Msumbiji Eusebio
Mbali na gwiji huyo wa ujerumani, mshambuliaji wa Ureno, Eusebio naye aliweka rekodi ya kufunga magoli 9 kwa kila msimu katika misimu mitatu mfululizo. Wengine ni Jose Augustino Torres 64-65 aliyekuwa na magoli tisa akicheza klabu ya Benfica pamoja na shujaa Eusebio na mwaka uliofuata mchezaji mwingine Ferencvaros Florian Albert aliandika historia yake kwa kupachika magoli matano.

Source; Kwa msaada wa Mtandao

Saturday, February 18, 2012

K-NEL AHABARISHA HASA KUHUSU ULAYA NA MAREKANI

 Mwanamuziki wa Rap na Mjasiriamali K-Nel akiwa mitamboni.
K-Nel ni mtangazaji wa kipindi cha Surprising Europe kinachorushwa hewani na runinga lililojizolea umaarufu duniani kwa kuanika uchafu wa mataifa yaliyoendelea Al-Jazeera ( Kisiwa) kilichokuwa na kitovu chake jijini Doha, Qatar mashariki ya kati.

Surprising Europe ni kipindi cheye chenye mlolongo wa habari za maisha ya waafrika waliohamia Ulaya na Marekani kihalali au kiharamu, na kuwaonyesha namna wamatumbi wanavyohangaika usiku na mchana wakisoma vyuo na kutafuta maisha kijumla huku wakipambana na hali ngumu ya uchumi wa kiliberali, utamaduni, hali ya hewa, ubaguzi wa rangi na upweke.

Kipindi kinachimba shimo kubwa hasa kwa kuwamulika waafrika na matatizo, mashakili na masaibu yao wakiwa katika nchi hizo za barafu na baridi kali zenye utofauti mkubwa na bara la afrika. Waafrika wanaonyeshwa namna wanavyofanya kazi chafu na za kidhalimu na kidhalili huku kipato chao kikishindwa kukidhi mahitaji ya kila siku, waafrika wanajiuza, wanasafisha vyoo, barabara, wanatembeza bidhaa, wanasuka nywele wazungu kwenye fukwe za bahari, wahudumu wa baa, wengine wakijihusisha na uuzaji wa dawa za kulevya na kuhatarisha maisha yao ili mradi mkono uende kinywani.

Pia kinahabarisha namna baadhi ya wamatumbi wanavyobaka na kufoji hati za kuishi ili wasisumbuliwe.
Surprising Europe ni kipindi elimu hasa kwa wote wenye ndoto za kwenda majuu kwa mintaarafu ya elimu, kutafuta maisha na bahati kadhalika za Dunia hii.

Alizaliwa jijini Nairobi, Kenya kama Nelson Mike Mithambo Miriuki kuanza mambo ya kunga ya uimbaji akiwa kinda wa miaka 4 akiimba nyimbo za kwaya, kuandika tamthiliya ndogo na mashairi.

Alipokuwa tineja akaingiwa na mdudu wa RnB na Hip Hop na kuwahusudu sana wanamuziki wa kimarekani marehemu Tupac Shakur, Big Poppa na shujaa wake wa muziki Jay Z.

K-Nel alihamia Ujerumani akiwa na miaka 19 kwa dhamira ya masomo ya Chuo Kikuu na mwaka 2004 na kuungana na Mama yake ambaye alikuwa akiishi huko muda mrefu. Alipakuwa jikoni albamu yake ya kwanza aliyoiita The Middle Finger na kubahatika kufanya kazi na msanii wa marekani Jay Z katika sherehe za sikukuu ya uhuru wa Kenya zilizofanyika Cologne mwaka huo.

Akiwa na kofia takribani tatu, utangazaji, muziki na ujasiriamali K-Nel anawaeleza waafrika wote wenye ndoto za kwenda majuu kuwa hawana budi kuarifiwa kabla hawajafunga mikanda yao kwani si kila ving'aavyo ni dhahabu.

Anauma na kupuliza kwani kauli mbiu yake kwa wamatumbi wanaohusudu Ulaya na Marekani ni kuwa

kwa maelezo zaidi... www.surprisingeurope.com

Friday, February 17, 2012

MNAIJERIA UMAR MUTALLAB AFUNGWA JELA MAISHA

Kijana Umar akiwa ameweka pozi pembezoni mwa ukingo wa Mto Thames jijini London.
Akiwa bado kinda na kijana wa miaka 25, na shahada yake ya Uhandisi kutoka katika moja ya chuo kikuu kikongwe na maarufu cha UCL University College London alikohitimu jiwe lake hilo June, 2008, Kijana mtanashati, msomi kutoka katika familia ya kitajiri nchini Nigeria Umar Farouk Mutallab atatumia kudra alizojaliwa na Rabuka akiwa gerezani, kifungoni nchini Marekani.

Chupi iliyokuwa na bomu lililoshinda kuwasha kibiriti.
Umar alitaka kuishangaza dunia kwa kitendo chake cha kigaidi baada ya jaribio lake kushindwa kufua dafu Dec, 25, 2009 alipokuwa katika pipa lililokuwa linatoka jijini Amsterdam, Uholanzi na kukata mbingu ya Mungu kuelekea kwa Rais Obama katika jimbo la Michigan, Detroit ambapo lengo lilikuwa ni kuona safari yao ikigeuka majivu na watu kusaga meno huku maswahiba wakifurahi lakini Mungu si Athuman kwani kilipuko alichovaa katika kufuli kilishindwa kutimiza lengo lake baada ya wakaguzi wa ndege kumshukia kwa kuwa hakuwa katika hali ya utulivu.

Aliivaa chupi ambayo aliitegesha bomu ambalo lilishindwa kulipuka kwa manusura ya Mungu na kuokoa maisha ya abiria wapatao 253 katika ndege hiyo ya Northwest Flight Airlines

Kijana huyo wa Mutallab alijulikana kwa jina la Underwear Bomber kutokana na mkasa huo alihukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya kukutwa na mashtaka nane ya kigaidi. Hukumu hiyo ambayo imwashtua wazazi wake na kuwapa wahka wakidai kuwa mahakama haina budi kufikiria upya uamuzi waliofanya kwa kijana wao kwa kosa hilo la kibinadamu.

Wakati akisoma hukumu hiyo siku ya alhamisi ya feb 16, 2012, Jaji wa Mahakama ya Wilaya ya Detroit Nancy Edmunds amesema kuwa Umar anastahili hukumu hiyo kutokana na kitendo hicho cha kigaidi.

Umar angekutwa na adhabu ya kifo laiti jaribio lake lingeng'arimu hata maisha ya abiria mmoja ilhali hukumu hiyo itaendana na ukosefu wa msamaha wa Rais yani Parole.

Thursday, September 8, 2011

"Hujafa Hujaumbika"- Wasemavyo Wahenga

Bwana Tony Nicklinson alivyo sasa
     Tony Nicklinson amepooza kuanzia kwenye shingo, baada ya kuugua kiharusi tangu mwaka 2005 alipokuwa safarini kibiashara nchini Austria.
Bwana Nicklinson amekuwa ni mtu wa kukaa ndani kutwa kuchwa hukumwili wake ukiwa hauwezi kusogea kwenda mahali popote isipokuwa akili yake ndo inayoendelea kufanya kazi kwa kuweza kuzungusha macho ya kutikisa kichwa basi.

     Tony ambaye alikuwa ni Mhandisi huishi na mkewe Bibi Jane Nicklinson ambaye ndiye anayemsaidia kwa kumuogesha, kumvalisha na kumlisha huku akimwendesha katika baiskeli ya walemavu  na pia kumwekea kisanduku cha herufi kiitwacho Perspex Box atakapo kuongea jambo na maneno yale huandikwa katika kifaa maalum wa njia ya ujumbe

   Ana umri wa miaka 57 sasa na amekuwa akiuguzwa nyumbani kwake kwa takribani miaka sita huku akilaumu kuwa amechoshwa na maisha yake kwani anahisi ni mateso na anapenda sheria za Uingereza zinabadilishwa ili aweze hata kuuawa ili apate kupumzika Right of Private Life au Suicide Legal
Sheria nchini Ungereza haziruhusu mtu kujiua, hivyo bwana Nicklinson amekuwa akishutumu sheria hiyo kuwa humnyima mtu uhuru wa kutotaka kuendelea kuishi.

    Akijibu swali hilo kwa mwandishi wa habari wa BBC Stephen Tackur kupitia kipini cha mahojiano cha Hardtalk  Bi Jane Nicklinson amesema kuwa endapo sheria hiyo haitapitishwa nchini humo basi hatokuwa na budi kwenda nchini Switzerland ambapo  mumewe ataweza kuruhusiwa  kufanyiwa Mercy Kiling ili kuepuka adha na fadhaa anazoendelea kuzipata mumewe huyo aliyebarikiwa kupata naye watoto wakike wawili ambao wanajitegemea
Mke wa bw. Nicklinson Jane Nicklinson
Bi Jane pia amekiri katika mahojiano hayo kuwa yu tayari kumuona mumewe akiuawa kwani maisha yake humpa huzuni na majonzi sana akikumbuka kipindi alipokuwa mzima wakisafiri pamoja ulimwenguni kote, hakika humuumiza sana mtima wake.

   Pomoja na kupooza ila Bwana Nicklinson  anaandika historia ya maisha  yake ( MEMOIRS) kabla hajapata kupooza na mapaka sasa alivyo.
Bwana Tony Nicklinson anaishi na mkewe mpendwa Bi Jane Nicklinson kwa miaka 24 sasa na wana mabinti wawili Lauren 22 na Beth  21 wote wakiishi huko Chippenham, Wiltshire.

    Tony Niclinson alikuwa meneja wa ukakiki wa ubora katika Kampuni la Uhandisi la Ugiriki lililokuwa likifanya shughuli zake  katika nchi za jumuiya za falme za kiarabu (UAE) wanadai alikuwa mchapakazi na mwenye nguvu.


    Maisha ya Bwana Tony Nicklinson hutukumbusha methali ya Wahenga inenayo kuwa “ Hujafa Hujaumbika Mwana-adam”

    Source: Hard Talk,  BBC World Service